EU kutumia kikosi maalum kuzuia wahamiaji

Wahamiaji
Image caption Idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya imeongezeka sana mwaka huu

Viongozi wa muungano wa Ulaya, wamesema kuwa wataharakisha juhudi za kuunda kikosi cha pamoja cha kulinda maeneo ya mipaka na bahari katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Rais wa baraza la muungano huo Donald Tusk, amesema mpango huo unatarajiwa kukamilika kufikia mwisho wa Julai mwaka ujao.

Kikosi hicho kitakuwa na majukumu zaidi ka kikosi cha sasa cha pamoja cha Frontex, ambacho kinasemekana kukosa vifaa vya rasilimali za kutosha kupamabana na tatizo la wahamiaji.

Mwaka huu pekee idadi kubwa ya wahamiaji wamevuka mipaka na kuingia Italia na Ugiriki wakitumia mashua

Ugiriki ndiyo tatizo kubwa zaidi kwa Muungano wa Ulaya, kwa sababu wahamiaji wengi wanasafiri kupitia nchi hiyo kabla ya kusajiliwa rasmi.

Taifa la Hungary ndilo lililokuwa la kwanza kujenga ukuta katika mpaka wake ili kuzuia wahamiaji kuingia, na tangu wakati huo mataifa mengi nayo yameanza kufuata mfano huo wa kujenga ua.

Kuanza kutekelezwa kwa vizuizi katika mipaka kumeathiri sana uhuru wa kutumiwa kwa sera ya Schengen ya uhuru wa kusafiri.

Wasiwasi kuhusu kanda inayotumia visa hiyo ya Schengen, yenye mataifa 26, na ambayo hayana ukaguzi katika maeneo ya mipakani, ulitawala mkutano huo wa Brussels.

BwTusk amesema wanachama wa muungano huo wa EU wameshindwa kulinda maeneo ya mipakani.

Lakini amesema baada ya mazungumzo hayo viongozi wa kanda hiyo inayotumia hati ya kusafiria ya Schengen, watakuwa makini zaidi katika maeneo ya mipakani.

Aidha amesema maafisa zaidi wa kikosi cha sasa cha Frontex watatumwa nchini Ugiriki baadaye mwezi huu.