Jaribio la mapinduzi latibuliwa Niger

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Issoufou alichaguliwa 2011 na kuhitimisha uongozi wa kijeshi wa miaka mingi

Rais wa Niger Mahamadou Issoufou amesema serikali yake imetibua njama ya kupindua serikali.

Bw Issoufou amesema waliopanga njama hiyo waliwa wamepanga kutumia “mashambulizi ya angani” kumuondoa madarakani.

Amesema hayo kwenye hotuba ya moja kwa moja kupitia runinga ya taifa.

Alichaguliwa 2011, na kuhitimisha miaka mingi ya utawala wa kijeshi.

Niger imeshuhudia mapinduzi kadha ya serikali tangu kujipatia uhuru 1960.

Wasiwasi unaongezeka kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ambao Issoufou anatarajiwa kushinda.

„Serikali imetibua jarabio la kuvuruga uthabiti wa nchi. Lengo la watu hawa, ambao sijui wanachochewa na nini, lilikuwa kupindua serikali iliyochaguliwa na raia,” amesema.

Maafisa wanne wakuu wa jeshi wamekamatwa, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti, lakini haijabainika ni kwa nini wakakamatwa.

Muda mfupi baada ya Issoufou kuchaguliwa 2011, maafisa 10 wa jeshi walikamatwa wakidaiwa kupanga jaribio la kumuua.