Putin atumia lugha chafu kushutumu Uturuki

Putin Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Putin amesema haoni matumaini yoyote ya kufufuliwa kwa uhusiano na Uturuki

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametumia lugha chafu akishambulia tena Uturuki kwa kuidungua ndege ya kivita ya Urusi mwezi uliopita.

“Waturuki”, amesema, wameamua “kuramba Wamarekani pahala fulani”.

Alisema hayo alipokuwa akihutubu kwenye kikao cha kila mwaka cha kuwahutubia wanahabari.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa urais Marekani mwaka ujao, kiongozi huyo wa Urusi alimtaja mgombea wa chama cha Republican Donald Trump kuwa "mtu mchangamfu, na mwenye kipaji” na "anayeongoza kinyang’anyiro cha kuwania urais”.

Bw Putin kwa sasa yumo kwenye muhula wake wa tatu tangu 2000, na taifa hilo linakabiliwa na mzozo wa kiuchumi.

Wakosoaji wa utawala wake wanasema haki za raia zimekandamizwa wakati wa utawala wake.

Anasalia mmoja wa wanasiasa wasifika duniani na aliongoza kwenye orodha ya jarida la Forbes ya Watu Mashuhuri na Wenye Ushawishi Duniani kwa mwaka wa tatu mtawalia.

Urusi ilituma majeshi yake Syria mwezi Septemba kusaidia Rais Bashar al-Assad na ndege za kivita za Urusi zimekuwa zikishambulia ngome za wapinzani wa Assad.

Hatua ya Urusi imekosolewa vikali na Uturuki, Marekani nan chi za Ghuba ya Uarabuni.

Bw Putin alisema kuangushwa kwa ndege ya kivita ya Urusi na majeshi ya Uturuki karibu na mpaka wa Syria na Uturuki ulikuwa “uchokozi” lakini Urusi si taifa la “kusalimu amri” na kutoroka.

Alisema kwa sasa haoni matumaini yoyote ya kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na Urusi chini ya viongozi wa sasa.

Urusi tayari imewekea Uturuki vikwazo.