Urusi: Habari muhimu kuhusu ndege ziliharibiwa

Putin Haki miliki ya picha EPA
Image caption Putin ameionya Uturuki kwamba itajuta kudungua ndege hiyo

Kadi ya kunakili kumbukumbu katika kifaa maalum cha kunakili sauti kwenye ndege maarufu kama Black Box, ya ndege ya kivita ya Urusi iliyodunguliwa katika mpaka wa Syria mwezi uliopita iliharibiwa kabisa, haya ni kwa mujibu wa wachunguzi kutoka Urusi.

Kifaa hicho cha ndege hiyo yenye usajili Su-24, kilifunguliwa rasmi mjini Moscow mapema hii leo mbele ya waandishi wa habari na mabalozi.

Afisa mkuu wa jopo hilo la wachunguzi kutoka Urusi, Nikolai Primak, amesema kuwa habari zilizokuwa zimenakiliwa na kifaa hicho havipo.

Data kutoka kwa kifaa hicho kingesaidia kutatua mzozo kuhusu mahala ndege hiyo ilikokuwa wakati ilipodunguliwa.

Matokeo ya uchunguzi wa kina wa kifaa hicho yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

Kuangushwa kwa ndege hiyo kuliharibu uhusiano kati ya Urusi na Uturuki, hali iliyoifanya Urusi kuiwekea Uturuki vikwazo.

Uturuki imekariri kuwa ndege hiyo inayomilikiwa na jeshi la Urusi, iliyotumwa nchini Syria kuunga mkono utawala wa Bashar al-Assad, ilipuuza onyo ya kuondoka katika anga yake.

Lakini Urusi imesema ndege hiyo iliangushwa ikiwa ndani ya anga ya Syria, na rais wa Urusi, Vladimir Putin alionyesha tena ghadhabu zake dhidi ya Uturuki kwa kuishutumu kwa kushirikiana na Marekani kukuza dhana ya kusambaa kwa Uislamu wenye itikadi kali.