Muungano wa Marekani waua wanajeshi wa Iraq

IS Haki miliki ya picha AP
Image caption Vikosi vya Iraq vimekuwa vikishambulia maeneo yanayodhibitiwa na IS

Shambulio la angani la majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya wapiganaji wa Islamic State (IS) huenda liliwaua wanajeshi wa Iraq, jeshi la Marekani limesema.

"Ripoti za awali zinaonyesha uwezekano kwamba shambulio moja lilisababisha vifo vya wanajeshi wa Iraq,” taarifa ya jeshi la Marekani ilisema.

Afisa mmoja na wanajeshi tisa waliuawa au wakajeruhiwa kwenye kisa hicho, wakuu wa jeshi la Iraq nao wamesema.

Majeshi ya Iraq yamekuwa wakikabiliana na wapiganaji mkoa wa Anbar.

Shambulio hilo la angani lilitekelezwa karibu na mji wa Fallujah ambako majeshi ya Iraq yamekuwwa yakikabiliana na wapiganaji wa IS.

Kutokana na hali mbaya ya hewa, Iraq haikuweza kuwasaidia wanajeshi wake kwa ndege angani na ndiyo iliyoomba majeshi ya muungano kusaidia kwa mashambulio ya angani.

Mashambulio mawili ya kwanza yaliwezesha vikosi vya Iraq kusonga upesi, na la tatu lilipokuwa likitekelezwa halikuzingatia kwamba wanajeshi wa Iraq walikuwa wamepiga hatua na kuingia maeneo ambayo awali yalikuwa yamedhibitiwa na IS.

Jeshi la Marekani limesema hicho ni kisa cha kwanza cha aina hiyo katika Operesheni Inherent Resolve ambayo lengo lake ni kufurusha IS kutoka mkoa wa Anbar.