Uchina yaituhumu Marekani kwa “uchokozi”

China Haki miliki ya picha
Image caption Uchina imekuwa ikijenga visiwa bandia eneo hilo

Uchina imeituhumu Marekani kwa kufanya “uchokozi mkubwa” baada ya ndege ya Marekani aina ya B-52 kupaa karibu na visiwa vya Spratly, bahari ya South China.

Maafisa wa jeshi la Uchina waliwekwa kwenye “tahadhari ya hali ya juu” wakati wa kisa hicho kilichotokea tarehe 10 Desemba, na wakaagiza ndege hiyo kuondoka.

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema inachunguza malalamiko kutoka kwa Uchina.

Uchina inadai kumiliki maeneo makubwa ya bahari ya South China, maeneo ambayo mataifa yaliyo karibu pia yanadai kumiliki.

Mwezi Oktoba, Uchina iliikemea Marekani baada ya meli yake ya kivita kupitia karibu na visiwa hivyo.

Mnamo Jumamosi, taarifa kutoka wizara ya ulinzi ya Uchina iliituhumu Marekani kwa kuongeza wasiwasi eneo hilo makusudi kwa kutuma ndege ya kuangusha mabomu aina ya B-52 juu ya visiwa vya Spratly, ambavyo Uchina huviita Nansha.

Imetoa wito kwa Marekani kuzuia visa kama hivyo siku sijazo.

Marekani haijaegemea upande wowote kuhusu umiliki wa visiwa hivyo lakini hutumia sera ya "uhuru wa kupitia eneo fulani la kimataifa” katika kutetea kupita kwa ndege zake za kivita.

Msemaji wa Pentagon Kamanda Bill Urban hata hivyo amesema ndege hiyo B-52 haikuwa inatumia sera hiyo, jambo linaloashiria huenda ilipotea njia.