UNHCR yaonya kuhusu ongezeko la wakimbizi

Guterres Haki miliki ya picha AFP
Image caption Shirika hilo limesifu juhudi za EU lakini linasema hazitoshi

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi linasema kuwa idadi ya wakimbizi wanaolazimishwa kuondoka makwao kwa sababu ya vita imeongezeka sana mwaka huu.

Idadi hiyo inatarajiwa kuzidi milioni 60.

Taarifa hiyo ya UNHCR imetolewa wakati mashirika ya misaada mjini Geneva yanasema kuwa idadi ya watu wanaovuka bahari ya Mediterranean kuingia Ulaya mwaka huu itapita milioni moja.

Kwa mujibu wa shirika hilo, idadi ya watu waliotoroka makwao mwaka huu imeongezeka pakubwa na kuzidi ile ya wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

Mkuu wa shirika hilo Antonio Guterres amesema kuwa hali hiyo inahitaji uvumilivu, moyo wa huruma na umoja, hasa kwa bara la Ulaya, ambako maelfu ya watu, wengi wao kutoka Syria wanawasili kila siku.

Bw Guterres ametoa wito wa kuwepo kwa mpango wa kuwapatia makao wakimbizi, utakaohusisha maelfu kwa maelfu ya watu.

Hilo halitakuwa suala ambalo viongozi wa ulaya wangependa kulisikia.

Bado wamegawanyika kuhusiana ni nini la kufanya kuhusu idadi kubwa ya wakimbizi wanaoendelea kuwasili kwenye fukwe za nchi zao. Bw Guterres hata hivyo amesifu hatua ya Muungano wa Ulaya ya kuharakisha uchunguzi wa wahamiaji nchini Ugiriki, lakini akasema haitoshi.