Gavana aomba msaada wa rais kupitia Facebook

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Afisa huyo Mohammad Jan Rasoulyar alimwandikia rais Ashraf Ghani kumweleza kuwa wanajeshi 90 wameuawa katika mapigano makali na wanamgambo wa Taliban

Naibu gavana wa jimbo la Helmand Kusini mwa Afghanistan amewashangaza wengi kwa kumuandikia rais wa Afghanistan barua kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Afisa huyo Mohammad Jan Rasoulyar alimwandikia rais Ashraf Ghani kumweleza kuwa wanajeshi 90 wameuawa katika mapigano makali na wanamgambo wa Taliban, katika muda wa siku mbili zilizopita.

Bwana Rasoulyar, pia amesema kuwa wilaya tatu tayari zimedhibitiwa na Taliban, ilihali wilaya nyingine mbili imo katika hatari ya kutwaliwa.

Bwana Rasoulyar amelalamika kuwa hakuna uungwaji mkono kutoka kwa utawala mjini Kabul huku akimuomba Rais Ashraf Ghani kuchukua hatua za haraka kuzuia maafa zaidi.

Aidha alisema kuwa rais Ghani alikuwa anafichwa ukweli halisi wa mambo.

''Nakiri kuwa Facebook sio njia mahsusi ya kuwasilisha ujumbe ila sikuwa na njia mbadala ya kukutahadharisha kuwa "Helmand iko katika hatari ya kutwaliwa na adui.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Gavana aomba msaada wa rais kupitia Facebook

''Ninafahamu kuwa hapa sio kama Kunduz, ambapo serikali itaendesha kampeini kali ya kupambana na maadui kunusuru uwanja wa ndege hapa hilo haliwezekani'' alielezea naibu gavana.

Bwana Rasoulyar alimuomba rais Ghani kuingilia kati ilikuokoa kanda yake.

"Kila mmoja wetu anapenda madaraka nami si tofauti.

''Ninapenda kazi yangu ''

''Hata hivyo sitaweza kujitolea kufa kwa sababu ya kazi hii '' alisema Rasoulyar.

Image caption ''Tafadhali nakuomba uiokoe Helmand kutokana na athari ya kuangamizwa''.

''Tafadhali nakuomba uiokoe Helmand kutokana na athari ya kuangamizwa''.

Nakusihi ujiepushe na hao mawakili wanaokuzunguka na kukueleza kuwa kila kitu ki shwari ,la si ukweli hali ni mbaya sana''.

Waraka huo wake kulingana na mwandishi wa BBC wa maswala ya Asia Kusini Ethirajan Anbarasan inadhihirisha hali ilivyotete.