Air France: Hatukujua mauti imetuandama abiria

Image caption Air France: Hatukujua mauti imetuandama abiria

Abiria mmoja aliyekuwa katika ndege ya Ufaransa ya Air France AF463 anasema kuwa hawakuelezwa kwa nini ndege hiyo ilikuwa imebadili mkondo na kuelekea Mombasa Kenya badala ya uwanja wa Charles de Gaulle ulioko Paris.

Benoit Lucchini alisema kuwa waligundua ''ndege hiyo ilikuwa ikitua kwa utaratibu na wakadhania kuwa ilikuwa imepata hitilafu ya kimitambo''.

''Mimi na wenzangu tuliona ndege ikitua kwa utaratibu tu.''

''Kisha tukangudua ilikuwa inaelekea Mombasa Kenya na tukadhania kuwa labda ni hitilafu ya kimitambo.''

''Cha kushtaajabisha ni kuwa wahudumu wote wa ndege hiyo walikuwa wakarimu na watulivu mno.''

''Wala hawakuonesha ishara yeyote ya hofu wala taharuki.''

Kwa hakika hatukujua kilichokuwa kikiendelea'' alisema bwana Lucchini muda mchache baada ya kutua Mombasa.

Image caption ''Wala hawakuonesha ishara yeyote ya hofu wala taharuki.''

Polisi nchini Kenya wanasema tahadhari zote zilichukuliwa baada ya rubani wa ndege hiyo ya Ufaransa AF463 alipoomba ruhusa ya kutua kwa dharura akitokea Mauritius.

Wakati huo ndipo walipofahamishwa kuwa kulikuwa na kifurushi ndani ya choo cha ndege hiyo.

Abiria wote waliokolewa salama.

Kwa sasa Mamlaka inayosimamia usafiri wa ndege imetenga ndege hiyo na kuondoa kifurushi hicho kinachodhaniwa kuwa kilipuzi.

Msemaji wa polisi nchini Kenya Charles Owino anasema kuwa uchunguzi unaendelea na kuwa shughuli za kawaida zimerejea katika uwanja huo ambao ni maarufu kwa watalii wanaokwenda likizoni.