FIFA: Blatter na Platini nje kwa miaka 8

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Blatter na Platini nje kwa mika 8

Maafisa wawili wakuu zaidi katika usimamizi wa kandanda duniani rais Sepp Blatter na mwenyekiti wa shirikisho la soka barani ulaya UEFA Michel Platini, wamepigwa marufuku ya miaka 8 ya kutoshiriki kwa vyovyote maswala ya soka kufuatia uchunguzi wa kimaadili.

Wamepatikana na hatia ya ukiukaji wa maswala mbalimbali kama vile kashfa ya dola milioni mbili malipo yasiyo rasmi ambazo zilikabidhiwa Patini mwaka 2011.

Maafisa hao wawili wanasisitiza kutofanya makosa yoyote.

Marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja.

Rais huyo wa Fifa tangu mwaka 1998, Bwana Blatter, mwenye umri wa miaka 79, tayari ametangaza kujiondoa katika kinyanganyiro cha kumtafuta rais mpya wakati wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo mwezi Februari mwakani.

Naye nahodha wa zamani wa Ufaransa Platini, mwenye umri wa miaka 60, na ambaye alionekana kama kiongozi wa baadaye wa shirikisho hilo, amekuwa akipigiwa upatu wa kuchukua mahala pa Blatter katika uchaguzi mkuu unaopangiwa kufanyika Februari mwakani.

Bingwa huyo mara tatu wa mchezaji bora wa mwaka wa bara Ulaya na nahodha wa zamani wa Ufaransa, amekuwa Rais wa UEFA tangu mwaka 2007.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Viongozi hao wote wawili wanapania kukata rufaa mahakamani.

Kauli hii ya kamati ya maadili inaonekana kukatiza taaluma yao katika kandanda .

Blatter na Platini pia wamepigwa marufukuya dola elfu arobaini ($40,000) na ($80,000) mtawalia.

Blatter amesema kuwa atakwenda katika mahakama ya maswala ya michezo (Court of Arbitration for Sport) iliyoko Lausanne kukata rufaa.

Blatter anasema kuwa malipo hayo yalikuwa ya kazi aliyomfanyia lakini kamati ya uadilifu na nidhamu ya FIFA imewapata na hatia ya kuwa yalikuwa malipo ya kiinua mgongo.

Kamati ya uadilifu na nidhamu hata hivyo imewapata na hatia ya kutoa pesa na kuingia katika kandarasi kinyume na maadili ya FIFA.