Mfalme wa Afrika Kusini kuanza kifungo leo

Haki miliki ya picha
Image caption Mfalme wa Afrika Kusini kuanza kutumikia kifungo leo

Serikali ya Afrika Kusini inatarajia mfalme wa kabila la aliyekuwa rais Nelson Mandela, la Thembu, kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 gerezani hii leo.

Kauli hiyo inafuatia mahakama ya kikatiba kufutilia mbali ombi lake la kuaka kesi yake isikizwe upya.

Mfalme huyo , Buyelekhaya Dalindyebo alipatikana na hati ya utekaji nyara, kutekeleza shambulizi na uteketezaji wa mali.

Hii ni hata baada ya mawakili wa mfalme Dalindyebo kutuma ombi kwa wizara hiyo wakitaka kesi hiyo irejelewe upya.

Kulingana na msemaji wa wizara ya haki, Waziri anayehusika Michael Masutha analishughulikia ombi hilo, japo agizo lililotolewa na mahakama - linalomtaka mfalme huyo kuenda mahakamani kufikia mwisho wa siku - bado halijafutwa.

" waziri hajaarifiwa lolote kuhusu ubadilishaji wowote kuhusu agizo la mahakama" msemaji wa wizara ya haki, bwana Mhaga amesema.

Chini ya sheria za Africa Kusini, kesi hiyo huenda ikarejelewa iwapo ushahidi mpya utachipuka.

Kesi hiyo inahusu mzozo ulioibuka kati yake na baadhi ya watu anaowaongoza yapata miongo miwili ilopita.

"Tabia yake (mfalme Dalindyebo) ilikuwa inasikitisha sana kwa sababu waathiriwa wa uongozi wake wa vitisho, walikuwa walala hoi, waliokuwa wakimtegemea.

''Katiba yetu haikubali tabia kama hiyo".Jaji wa mahakama kuu zaidi alisema akitoa hukumu yake mwezi oktoba.