Ukame wasababisha giza kutawala Zambia

Haki miliki ya picha james jeffery
Image caption Zambia yabakia gizani kufuatia mgao wa umeme

Huku siku kuu ya Krismasi na mwaka mpya ikikaribia, maeneo mengi nchini Zambia yameachwa gizani baada ya taifa hilo kukumbwa na ukosefu wa umeme.

Hayo yamesemwa na waziri wa kawi Dora Siliya.

Katika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook, Waziri Dora Siliya amesema kuwa kupotea kwa umeme kumetokana na muundo msingi uliyoharibika.

Aidha waziri Dora amesema maeneo yatakayoathirika ni mikoa ya Kusini na Magharibi mwa taifa.

Image caption Lakini eneo la bwawa la Victoria Falls na viunga vyake hayajaathirika

Majimbo hayo yanapata umeme unaozalishwa kwa nguvu za maji kutoka katika bwawa la Victoria Falls.

Lakini eneo la bwawa la Victoria Falls na viunga vyake hayajaathirika

Kisa hiki cha sasa cha kupotea kwa umeme ni sawa na kilichofanyika Disemba 11 mwaka huu.

Zaidi ya watu laki moja u nusu katika mji mkuu Lusaka, wanakosa huduma ya umeme baada ya uhaba mkubwa wa mvua tangu Oktoba mwaka jana hadi Machi mwaka huu.

Image caption Wakati mwengine serikali inalazimika kutoa umeme kwa mgao kwa hadi saa 14 kwa siku.

Ukosefu huo wa mvua umesababisha kuwepo kwa kiwango kidogo mno cha maji katika mabwawa yanayozalisha umeme na kusababisha tatizo hili linaloshuhudiwa sasa la kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme.

Wakati mwengine serikali inalazimika kutoa umeme kwa mgao kwa hadi saa 14 kwa siku.

Awali Zambia ilifahamika kama taifa ambalo uchumi wake unakuwa kwa kasi mno barani Afrika na kufikia asilimi 7 kila mwaka katiika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hasa kutokana na uchimbaji madini ya shaba nyekundu na madini mengine.