Utafiti: Mimba nyingi hutungwa Krismasi

Haki miliki ya picha Thinkstock

Utathmini wa takwimu kuhusu watoto wanaozaliwa Uingereza umebaini mimba nyingi hutungwa wakati wa Krismasi kuliko wakati mwingine wowote ule wa mwaka.

Takwimu hizo za kipindi cha miongo miwili kutoka Idara ya Taifa ya Takwimu zinaonyesha watoto wanaozaliwa huongezeka sana wiki 40 (miezi 9) baada ya msimu wa sikukuu.

Hili huenda linatokana na wanandoa kutumia muda mwingi pamoja wakisherehekea, au kulenga makusudi mwanzo wa mwaka mpya wa shule ambao huanza mapema Septemba nchini humo.

“Ongezeko la watoto wanaozaliwa mwishoni mwa Septemba ni ishara kwamba mimba nyingi hutungwa wiki chache kabla ya Krismasi na kuendelea hadi siku chache baada ya Krismasi kuliko wakati mwingine wowote wa mwaka,” idara hiyo imesema.

Kawaida watoto 1,800 huzaliwa kila siku lakini idadi hii hupanda hadi 1,974 siku yenye kuzaliwa watoto wengi zaidi ambayo ni Septemba 26.

Siku zinazoshuhudia idadi ndogo zaidi ya watoto wanaozaliwa ni siku za Krismasi, Boxing Dei na siku ya Mwaka Mpya.

Hili sana huenda linatokana na idadi ndogo ya watu wanaopangiwa kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji siku hizo, kwani huwa ni siku za mapumziko.

Profesa wa masuala ya uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield Allan Pacey ameambia BBC: “Wazo kwamba mimba nyingi hutungwa wakati wa Krismasi lina msingi. Nina uhakika sherehe na shamra shamra za wakati huu huchangia.”