Wengi wafariki kwenye mlipuko wa gesi Nigeria

Watu wengi wamefariki baada ya mlipuko kutokea katika kiwanda cha gesi kusini mashariki mwa Nigeria.

Mlipuko ulitokea lori lilipokuwa likitolewa gesi ya kupikia aina ya butane katika mji wa Nnewi katika jimbo la Anambra.

Idadi ya waliofariki inatofautiana, baadhi ya ripoti zikisema waliofariki ni 35 na nyingine kwamba waliofariki wanafikia watu 100.

Waliofariki ni pamoja na wafanyakazi wa kiwanda na majirani.

Polisi wa eneo hilo wamethibitisha kisa hicho lakini hawajatoa maelezo zaidi.

Moto mkubwa ulitokea baada ya mlipuko.

Waliofariki na wajeruhi walipelekwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Nnamdi Azikiwe mjini Nnewi, ambao una Wakristo wengi.

Chukwuemerie Uduchukwu, aliyeshuhudia kisa hicho, ameambia BBC kwamba watu walikuwa wamefika kiwandani kununua gesi wakijiandaa kwa mapishi wakati wa Krismasi.

Alisema miili mingi ya wateja na wafanyakazi wa kiwanda hicho ilichomeka kiasi cha kutotambulika.

Mlipuko ulikuwa mkubwa kiasi kwamba nyumba zilizo karibu pia ziliharibiwa.

"Saa tano baada ya mlipuko, moto ulikuwa bado unawake huku maafisa wa msalaba mwekundu na wazimamoto wakiwa bado eneo hilo wakitafuta manusura,” amesema Bw Uduchukwu.

Mwandishi wa habari wa shirika la Associated Press amesema alihesabu miili ya watu 100.

Mtu mwingine aliyeshuhudia ameambia gazti la Vanguard kwamba mlipuko ulitokea lori lilipoanza kutoa gesi bila kusubiri muda unaohitajika joto la gari kupungua.

Wapita njia pia waliathiriwa na mlipuko huo, gazeti hilo limeripoti.

Walioshuhudia wanasema kulitokea moto mkubwa na moshi mweusi ukatanda kote angani eneo hilo.