Kiir aidhinisha majimbo mapya Sudan Kusini

Upinzani
Image caption Upinzani umesema majimbo hayo mapya yanaigawanya Sudan Kusini kwa misingi ya kikabila

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, ametoa ilani ya kuunda majimbo mengine 28, kutoka kwa yale kumi ya zamani.

Wachanganuzi wanasema kuwa hatua hiyo ya kushangaza inahujumu hatua ya kugawana mamlaka iliyokubaliwa chini ya muafaka wa amani ulioafikiwa mwezi Agosti mwaka huu.

Muafaka huo ulikuwa na nia ya kumaliza kabisa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Siku ya Jumatatu, waasi wapatao 150 walirejea katika mji mkuu - Juba, ili kuanza kuunda serikali ya mseto ya umoja wa kitaifa.

Wanasema kuwa sasa wanajadiliana kuhusiana na hatua gani watakayoichukua ambayo wanapania kutangaza Alhamisi ijayo.

Juma lililopita kundi moja la kimataifa linaloshughulikia mizozano ya dharura lilionya kuwa muafaka wa amani wa Sudan Kusini ni dhaifu kwani makundi mengi yaliyojihami, bado yanaunga mkono pande mbili hasimu.