Mwanaanga apiga ‘wrong number’ kutoka angani

Peake Haki miliki ya picha PA
Image caption Peake ndiye Mwingereza wa kwanza kwenda kituo cha ISS

Mwanaanga Tim Peake, ambaye ndiye Mwingereza wa kwanza kwenda kituo cha kimataifa cha anga za juu, ameomba msamaha baada ya kupiga nambari ya simu isiyo sahihi kutoka anga za juu.

Mwanaanga huyo aliandika ujumbe wake wa kuomba msamaha kwenye Twitter baada ya kumpigia simu mwanamke na kusema: "Hello, is this planet Earth?" (Hujambo, hii ni sayari ya dunia?).

Bw Peake amesema kwenye Twitter kwamba simu hiyo haikuwa ya mzaha.

Hata hivyo, hakusema ni nani hasa aliyekuwa akimpigia simu.

Peake, baba wa watoto wawili anayetoka Chichester, Sussex Magharibi, alitua katika kituo cha kimataifa cha anga za juu (ISS) Jumanne 15 Desemba.

Atakaa katika kituo hicho miezi sita akifanya utafiti wa kisayansi.

Mapema wiki hii, aliwasaidia wanaanga wenzake wawili kutoka nje ya kituo hicho.

Wanaanga Tim Kopra na Scott Kelly, kutoka kituo cha Nasa cha Marekani walihitaji kutoka nje ya kituo hicho kukarabati kifaa kilichokuwa kimeharibika.