Janet Jackson aahirisha ziara ya kimuziki

Janet Haki miliki ya picha AP
Image caption Unbreakable ni albamu ya 11 ya Janet Jackson

Mwanamuziki nyota kutoka Marekani Janet Jackson ameahirisha ziara yake ya kimuziki ya Unbreakable ili kufanyiwa upasuaji.

Jackson amesema madaktari wake wamemwambia anahitaji kufanyiwa upasuaji “haraka”.

“Nawasihi mniombee, na familia yangu na kampuni yote wakati huu mgumu,” mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 49 ameambia mashabiki kupitia ujumbe mtandaoni.

Hajasema anahitaji kufanyiwa upasuaji wapi.

Jackson alianza ziara ya sasa Agosti mjini Vancouver na alikuwa amepangiwa kuzuru miji ya Marekani, Canada na Ulaya kabla ya Juni mwaka ujayo.

Onyesho lake la muziki ambalo lingefuata lingekuwa mjini Denver, Colorado, 9 Januari.

Mwaka 2008, Jackson alifuta maonyesho kadha ya muziki baada ya kupata matatizo ya kiafya yanayohusiana na ugonjwa wa vertigo.

"Inaniuma sana kwamba ninalazimika kuahirisha ziara ya Unbreakable Tour," amesema, na kuongeza kuwa mashabiki wanafaa kuendelea kukaa na tiketi.

Amesema tarehe mpya za ziara yake zitatangazwa.

Unbreakable ndiyo albamu ya 11 ya Jackson na yake ya kwanza studioni tangu kifo cha nduguye Michael mwaka 2009.