Ukumbi wa Waislamu wavamiwa Corsica

Ajaccio Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ukumbi wa maombi uliharibiwa mjini Ajaccio

Kundi la watu limevamia na kuharibu ukumbi wa maombi wa Waislamu katika kisiwa cha Ufaransa cha Corsica katika kinachoonekana kuwa shambulio la kulipiza kisasi kushambuliwa kwa wazima moto kisiwani humo.

Maafisa wa serikali wanasema kundi ndogo la waandamanaji pia lilijaribu kuteketeza Koran katika mji mkuu wa kisiwa hicho Ajaccio.

Mamia ya watu walikuwa wamekusanyika katika mji huo mkuu kulalamikia kujeruhiwa kwa wazima moto wawili na afisa mmoja wa polisi Alhamisi.

Watatu hao walishambuliwa na vijana waliokuwa wamejifunika nyuso.

Serikali imeshutumu visa vyote viwili na kuahidi kuadhibu waliohusika.

Shirika la habari la AFP linasema baadhi ya waandamanaji walienda hadi eneo ambapo maafisa hao walishambuliwa na kuanza kuimba “Waarabu waondoke!” na “Hapa ni nyumbani.”

Baadaye, walishambulia ukumbi wa maombi wa Waislamu, wakapora na kuchoma kiasi baadhi ya vitabu, zikiwemo nakala za Koran.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls ametaja shambulio hilo kuwa “lisilokubalika”.

Baraza la Waislamu la Ufaransa pia limeshutumu ghasia hizo.

Ufaransa imeimarisha usalama wakati huu wa sikukuu ya Krismasi baada ya shambulio la 13 Novemba kusababisha vifo vya watu 130.