Wakuu wakamatwa kwa sababu ya rushwa Serbia

Serbia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Mkuu wa Serbia Aleksandar Vucic (kulia) ameanzisha mazungumzo kuhusu kujiunga na EU

Polisi nchini Serbia wamewakamata watu 79, akiwemo waziri wa zamani kwa tuhuma za ufisadi.

Hatua hiyo imetajwa kuwa kubwa zaidi katika juhudi za kukabiliana na ufisadi nchini humo.

Waziri wa masuala ya ndani Nebosja Stefanovic amesema wakuu kadha wa mashirika ya serikali, maafisa wawili wa zamani wa wizara ya masuala ya ndani na mameya wa sasa na wa zamani ni miongoni mwa waliokamatwa.

Wanatuhumiwa kuhusika katika wizi wa pesa zinazokisiwa kufikia dola za Kimarekani 70 milioni.

Waziri wa zamani Slobodan Milosavljevic ni mmoja wa waliokamatwa. Anadaiwa kutumia vibaya mamlaka alipokuwa waziri wa kilimo, misitu na maji Mei 2007 hadi Julai 2008 na pia alipokuwa mkuu wa chama cha wanabiashara 2004 hadi 2007.

Mkuu wa zamani wa taasisi ya kupambana na ufisadi Zorana Markovic pia anazuiliwa.

Polisi wanawasaka washukiwa wengine watano.

Washukiwa hao wamekamatwa wiki mbili baada ya Serbia na Muungano wa Ulaya kuanza majadilio ya kuiwezesha Serbia kujiunga na muungano huo.

Wengi wa waliokamatwa ni wafuasi wa chama cha upinzani cha Democratic Party. Viongozi wa chama hicho wanasema watu hao wamekamatwa kwa sababu za kisiasa.