Watu wawili wauawa Mandera

Watu wawili wamefariki na wengine watatu kujeruhiwa baada ya wanajeshi kufyatulia risasi gari moja mjini Mandera katika hali ya kutatanisha, ripoti zinasema.

Wanajeshi wamekuwa wakifanya operesheni kali mjini humo baada ya kuripotiwa kwa visa kadha vya mashambulio ya kigaidi siku za hivi karibuni.

Maafisa wanne wa polisi wameuawa kwenye mashambulio kadha katika mji huo ulioko kaskazini mashariki mwa Kenya katika kipindi cha wiki moja.

Wawili kati ya hao waliuawa Jumapili baada ya gari walimokuwa wakisafiria kulipuliwa katika barabara ya Elwak-Lafey.

Msemaji wa wizara ya usalama Kenya Bw Mwenda Njoka amesema maafisa wa usalama wamekuwa wakifanya “operesheni ya kawaida” ya kiusalama.

Haki miliki ya picha
Image caption Maafisa wa usalama wamekuwa wakifanya operesheni ya kiusalama kutokana na kuongezeka kwa mashambulio kutoka kwa al-Shabab

Habari kuhusu kilichotokea kabla ya wanajeshi kufyatua risasi zinakinzana.

Wakazi wanasema watatu hao walikwama baada ya gari lao kupata panchari na nyingine kwamba walikaidi agizo la maafisa wa usalama la kuwataka wasimame.

“Kulikuwa na gari kando mwa barabara na polisi waliokuwa wamejifunika nyuso zao walikiwa wakiwa kwenye gari na kuanza kufyatulia risasi gari hilo,” anasema Saat Abajana, mwakilishi wa wadi katika bunge la jimbo la Mandera.

“Waliua watu wawili na kujeruhi watatu. Kati ya waliojeruhiwa, wawili walikuwa nje ya gari.”

Maandamano yameripotiwa katika mji huo, wakazi wakilalamikia mauaji hayo.