Kimbunga chaua watu 43 Marekani

Majimbo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Majimbo mengi yametangaza hali ya tahadhari

Watu 43 wameuawa katika kipindi cha siku tano zilizopita kutokana na kimbunga maeneo ya kusini na magharibi mwa Marekani.

Mafuriko, upepo mkali na barafu vimeharibu mamia ya nyumba na biashara na kutatiza uchukuzi.

Idara ya taifa ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo imetoa tahadhari ya kutokea kwa vimbunga majimbo ya Texas, Arkansas, Louisiana, Oklahoma and Mississippi.

Magavana wa Missouri, Oklahoma, na New Mexico wametangaza hali ya tahadhari.

Katika jimbo la Illinois, watu watano, wawili wakiwa watoto, walisombwa na mafuriko wakiwa ndani ya gari lao.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Upepo umeharibu nyumba na magari maeneo mengi

Na katika jimbo la Texas, watu 11 waliuawa na kimbunga kilichoandamana na upepo mkali wa kasi ya hadi kilomita 300 kwa saa.

Nyumba nyingi zimeharibiwa jimbo la Texas na magari kuchotwa kutoka barabarani. Watu watano walifariki wakiwa ndani ya magari yao kwenye barabara kuu inayopitia mji wa Garland.

Afisa wa polisi Pedro Barineau amesema watu wengi waliokuwa wakiendesha magari hawakufanikiwa kupokea tahadhari iliyotolewa kuhusu kimbunga kilichokuwa njiani.

Kimbunga hicho kimeharibu nyumba, makanisa, na miti katika eneo la umbali wa kilomita 64.

"Ni uharibifu mkubwa. Ni wakati mbaya kupatwa na tufani kama hili, baada ya Krismasi,” amesema Bw Barineau.

Gavana wa Texas Greg Abbott amesema afisi yake imetangaza eneo la Dallas na maeneo matatu ya karibu kuwa maeneo ya mkasa.

Amewataka wakazi watahadhari zaidi.