Waziri mkuu wa Iraq aahidi kufurusha IS

Ramadi Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Abadi alihutubia taifa kupitia runinga baada ya majeshi yake kuukomboa mji wa Ramadi

Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi amesema wapiganaji wa Islamic State (IS) watafurushwa kutoka kwa maeneo yote nchini humo.

Hii ni baada ya wanajeshi kufanikiwa kuukomboa mji wa Ramadi kutoka kwa wapiganaji hao.

Kwenye hotuba kupitia runinga, Bw Abadi ameapa kuukomboa mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq, mji wa Mosul, akisema hilo litakuwa “pigo kubwa na la mwisho” kwa IS.

Marekani iyamesifu majeshi ya Iraq kwa kuukomboa mji wa Ramadi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema IS wamepata pito kubwa.

Wapiganaji hao wa Kiislamu waliuteka mji wa Ramadi mwezi Mei, kitendo kilicholiaibisha sana jeshi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mji wa Ramadi umeharibiwa vibaya kutokana na viki kadha za mapigano makali

Wanajeshi wa Iraq wamekuwa wakipigana kuukomboa mji huo ulioko kilomita 90 magharibi mwa Baghdad kwa wiki kadha.

Picha zilizoonyeshwa runingani Jumatatu ziliwaonyesha wanajeshi wakipandisha bendera ya Iraq kwenye afisi kuu ya serikali katikati mwa mji huo.

Msemaji wa jeshi Brigidia Jenerali Yahya Rasul amesema wanajeshi hao walikuwa “wameuokomboa” mji wa Ramadi katika ushindi wa kihistoria.

Haki miliki ya picha Reuters

Maafisa wa Iraq hawakutoa idadi yoyote kuhusu waliofariki kwenye vita hivyo.

"2016 utakuwa mwaka wa ushindi mkubwa na wa kabisa, pale Daesh (IS) watakapotimuliwa kutoka Iraq,” alisema Bw Abadi kwenye runinga.

"Twaja kuukomboa mji wa Mosul na hilo litakuwa pigo kubwa na la kuangamisa Daesh (nchini Iraq),” akaongeza.