Trump kutumia $2m kila wiki kwa kampeni

Trump Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump alikuwa awali ametangaza kwamba hatachangiwa pesa za kampeni

Mgombea wa urais Marekani anayetafuta tiketi ya chama cha Republican Donald Trump amesema anapanga kutumia $2m (£1.3m) kila wiki kwenye matangazo ya kampeni.

Bw Trump amesema atazindua matangazo kwa wingi majimbo ya Iowa, New Hampshire na South Carolina kabla ya kuanza kwa uchaguzi wa kuwateua watakaopeperusha bendera za vyama uchaguzini.

Amesema hayo huku gavana wa zamani wa New York George Pataki akijiondoa kutoka kinyang’anyiro cha kumteua mgombea wa urais wa chama cha Republican.

Ripoti zinasema amejiondoa baada ya kukosa kufanya vyema kwenye kura za maoni.

Bw Trump, ambaye ni tajiri mkubwa alikuwa awali amesema atafadhili kampeni yake kwa kutumia pesa zake binafsi.

Aidha, amesisitiza kwamba ametumia kiasi kidogo cha pesa kwenye kampeni kufikia sasa, ingawa ni yeye anayeongoza.

"Nitatumia angalau $2m kwa na labda hata zaidi,” Bw Trump amesema kupitia video iliyopeperushwa na kituo cha utangazaji cha CNN.

"Nitazindua matangazo Iowa, New Hampshire, South Carolina, na yatakuwa mengi."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Trump anaongoza kwenye kura za maoni miongoni mwa wanaotaka kuwania urais Marekani

Bw Trump amekabiliwa na shutuma mara kadha kutokana na matamshi yake tata. Majuzi alikemewa kwa kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani baada ya wanandoa wawili wa Kiislamu kuua watu 14 mjini San Bernardino jimbo la California.

Uchaguzi wa kuteua watakaopeperusha bendera za vyama utaanza Februari. Uchaguzi wenyewe utafanyika Novemba.