Ndege ya India yakatiza safari kwa sababu ya panya

Ndege Haki miliki ya picha Getty
Image caption Shirika la Air India limenunua ndege za kisasa kama hii (si iliyoathirika)

Ndege iliyokuwa safarini kutoka Mumbai kwenda London ililazimika kukatiza safari na kurejea uwanja wa ndege baada ya panya kuonekana ndani ya ndege hiyo.

Ndege hiyo nambari AI 131 ilikuwa imefika Iran pale panya alipoonekana na mmoja wa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo, ripoti zinasema.

Abiria waliendelea na safari yao kwa kutumia ndege nyingine.

Shirika la Air India limesema ndege hiyo itanyunyiziwa dawa ya kuua wadudu na kwamba uchunguzi unafanywa kuhusu madai hayo ya kupatikana kwa panya huyo.

Shirika hilo limesema wahandisi wa ndege wanaendelea na uchunguzi “ingawa haijathibitishwa iwapo ni kweli kulikuwa na panya.”

Maafisa wa shirika hilo wamesisitiza kwamba uamuzi wa kukatiza safari ulichukuliwa kwa maslahi ya usalama wa abiria.

Panya wanaweza kuwa hatari wakiwa ndani ya ndege kwani wanaweza kutafuna nyaya.