Ujerumani: Hakuna hatari ya shambulio Munich

Polisi Haki miliki ya picha EPA
Image caption Polisi hata hivyo wameendelea kushika doria

Maafisa wa Ujerumani wamesema hawajapata habari zozote za kuonyesha kwamba mji wa Munich umo hatarini ya kushambuliwa wakati wowote na magaidi.

Tamko hilo limetolewa baada ya vituo viwili vikuu vya reli mjini humo kufungwa mkesha wa siku ya Mwaka Mpya baada ya kupokea habari za ujasusi kuhusu mipango ya wapiganaji wa Islamic State kushambulia.

“Hali sasa imetulia,” amesema waziri wa masuala ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann.

Kituo kikuu cha treni cha mji wa Munich na kituo cha Pasing, vilifunguliwa tena mapema leo baada ya kufungwa kama tahadhari.

Polisi wamesema wanawasaka washukiwa “watano hadi saba” ambao wanaaminika kuwa wa asili ya Iraq au Syria.

Lakini hali ya tahadhari hapa ni “sawa na ilivyokuwa jana usiku”, alisema Bw Herrmann, akizungumza na kituo cha utangazaji cha serikali ya Bavaria kwa jina BR.

Aliongeza pia kwamba kwa jumla Ulaya inakabiliwa na hatari ya kushambuliwa.

Kuhusu tahadhari iliyofanya vituo vya treni kufungwa, Bw Herrmann amesema maafisa hawana habari za ufasaha kuhusu ni wapi shambulio lilipangiwa kutekelezwa na ni wakati gani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maafisa walifunga vituo viwili vikuu vya treni mjini Munich

Polisi wa ziada walitumwa Munich kutoka maeneo mengine ya Bavaria kama tahadhari.

Miji mingi Ulaya ilikuwa katika hali ya juu sana ya tahadhari kutokana na hofu ya kutokea kwa mashambulio ya kigadi baada ya washambuliaji wa kujitoa mhanga kuua watu 130 mjini Paris 13 Novemba mwaka uliopita.

Nchini Ufaransa polisi zaidi ya 100,000 walitumwa maeneo mbalimbali kudumisha usalama, huku sherehe ya ulipuaji wa fataki ikisitishwa mjini Paris.

Mjini Brussels, sherehe ya kulipua fataki pia haikufanyika.