Kundi ladai kuhusika kutatiza tovuti za BBC

BBC
Image caption Tovuti nyingi za BBC zilikumbwa na matatizo kwa saa kadha Alhamisi

Kundi moja linalosema limekuwa likikabiliana na shughuli za Islamic State (IS) mtandaoni limedai kuhusika katika kuvuruga tovuti za BBC Alhamisi.

Tovuti zote za BBC zilikumbwa na matatizo kwa saa kadha mkesha wa Mwaka mpya kutokana na kile mdokezi katika BBC anasema kilitokana na uvamizi ambao kwa Kiingereza huitwa "distributed denial of service".

Uvamizi huu hufanya ionekane kana kwamba watu wengi sana wanatembelea tovuti kiasi kwamba tovuti hulemewa na kutatizika.

Kundi hilo linalojiita New World Hacking, linasema lilitekeleza uvamizi huo kama njia ya kupima uwezo wake.

BBC haijathibitisha rasmi wala kukanusha iwapo matatizo hayo yalitokana na uvamizi huo.

Kundi hilo limeandikia mwandishi wa teknolojia wa BBC Rory Cellan-Jones kwenye Twitter: “Makao yetu ni Marekani, lakini tumekuwa tukijaribu kuangusha tovuti zinazohusiana na IS, na pia wanachama wa Isis.

“Wakati mwingine yale huwa twafanya si mema, lakini bila wadukuzi…nani atapambana na magaidi mtandaoni?” kundi hilo liliandika.

"Sababu yetu kulenga BBC ni kwa sababu tulitaka kuona uwezo was ava zetu.”

Awali, kundi hilo la New World Hacking lilikuwa limesema: "Tulikuwa tunafanya majaribio tu, hatukupanga kutatiza tovuti hizo kwa saa kadha. Sava zetu zina nguvu sana.”

Afisi ya mawasiliano ya BBC Jumamosi ilisema haitajibu madai ya kundi hilo.