Islamic State washambulia kambi ya jeshi Iraq

Jumapili Haki miliki ya picha AP
Image caption Majeshi ya serikali yaliukomboa mji wa Ramadi Jumapili

Wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS) wameshambulia kambi ya jeshi karibu na mji wa Ramadi, siku chache baada ya mji huo kukombolewa na wanajeshi wa serikali.

Msemaji wa jeshi amesema washambuliaji waliokuwa kwenye ndege lililotegwa mabomu na wengine waliovalia mikanda ya kujilipua walishiriki shambulio hilo.

Jeshi lilikabiliana nao likisaidiwa kutoka angani na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani.

Serikali ya Iraq ilitangaza kwamba ilikuwa imefanikiwa kuukomboa mji wa Ramadi kutoka kwa IS Jumapili.

Wapiganaji hao walikuwa wameushikilia mji huo mkubwa tangu Mei.

Shambulio la Ijumaa ndilo la karibuni zaidi kutekelezwa na IS dhidi ya wanajeshi wa Iraq tangu kukombolewa kwa Ramadi.

Mtathmini wa BBC anayeangazia masuala ya Mashariki ya Kati Sebastian Usher, anasema shambulio hilo linaonyesha kibarua ambacho majeshi ya serikali yanakabiliwa nacho kulinda mji wa Ramadi.