Afungiwa Twitter akidhaniwa kuwa mkuu wa IS

Twitter Haki miliki ya picha Getty
Image caption Twitter kawaida huwa haizungumzii hadharani masuala kuhusu watu binafsi

Mwanaharakati aliyehusika katika wimbi la mageuzi nchi za Kiarabu alifungiwa akaunti yake ya Twitter baada ya kudhaniwa alikuwa ndiye kiongozi wa Islamic State.

Akaunti ya Iyad El-Baghdadi ilifungwa kwa muda wa nusu saa.

Bw El-Baghdadi alikuwa ametambuliwa kimakosa kama kiongozi wa wapiganaji wanaojiita IS Abu Bakr al-Baghdadi na gazeti la Republika la Indonesia na jarida la New York Post.

Ana zaidi ya wafuasi 70,000 kwenye Twitter na mara kwa mara kushutumu IS.

Twitter haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na kisa hicho.

Majuzi, Twitter ilifanyia mabadiliko sheria zake kuhusu matusi na uenezaji chuki, katika juhudi za kulinda watumiaji wa mtandao.

Imekosolewa kwa kutotia juhudi za kutosha kukabiliana na waenezaji wa propaganda za IS.

Bw El Baghdadi ameambia BBC alipokea ujumbe kutoka kwa Twitter akijulishwa kwamba “alivunjaa sheria za mtandao huo lakini hakuambiwa kosa lenyewe.

Ameituhumu Twitter kwa ubaguzi wa rangi.

"Sidhani kuna nchi yoyote ya Kiarabu duniani ambayo haina familia yenye jina El-Baghdadi," aliandika baadaye kwenye Twitter.