Iran: ‘Kisasi cha Mungu’ kitakumba Saudia

Tehran Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji walichoma picha za watu wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia nje ya ubalozi wa Saudia Tehran

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran amesema Saudi Arabia itakumbana na “kisasi cha Mungu” kwa kumuua mhubiri maarufu wa Kishia.

Ayatollah Khamenei amemtaja Sheikh Nimr al-Nimr kama "mfia dini" aliyetenda mambo yake kwa Amani.

Sheikh Nimr ni mmoja wa watu 47 waliouawa Ijumaa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi.

Lakini Ayatollah Khamenei amesema mhubiri huyo aliuawa kwa kupinga viongozi wa Kisuni wa Sunni.

"Msomi huyu aliyedhulumiwa hakuwahi kamwe kuwahimiza watu wachukue silaha, na wala hakuhusika kwenye njama,” kiongozi huyo wa kidini ameandika kwenye Twitter.

"Kitendo pekee cha #SheikhNimr kilikuwa kuzungumza waziwazi," alisema, na kuongeza kwamba “damu ya mfia dini aliyedhulumiwa #SheikhNimr ambayo imemwagwa kwa njia isiyo ya haki itaathiri hali upesi na kisasi cha Mungu kitawakumba wanasiasa wa Saudi Arabia".

Sheikh Nimr alishiriki maandamano ya kupinga serikali Saudi Arabia ambayo yalitokea wakati wa wimbi la mageuzi katika nchi za Kiarabu kabla ya kukamatwa kwake 2012.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sheikh Nimr alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Saudi Arabia

Iran, ambayo imekuwa ikishindana na Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati, imeongoza jamii za Washia katika kushutumu kuuawa kwa mhubiri huyo.

Maandamano ya kulaani kitendo hicho yamefanyika mkoa wa Mashariki nchini Saudi Arabia ambao una Washia wengi pamoja nan chi za Iraq na Bahrain.

Mhubiri mkuu wa Washia nchini Iraq Ayatollah Ali al-Sistani ameeleza mauaji ya mhubiri huyo kama “uchokozi”.