Wanabalozi wa Iran watakiwa waondoke Saudia

Riyadh Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Abdel al-Jubeir alitangaza kusitishwa kwa uhusiano kati ya nchi hiyo na Iran Jumapili

Wanabalozi wa Iran walio Saudi Arabia wamepewa siku mbili wawe wameondoka nchini humo, huku mzozo kuhusu mauaji ya mhubiri wa Kishia ukizidi.

Serikali ya Saudi Arabia ilitangaza Jumapili kwamba ilikuwa imekatiza uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Iran.

Iran imeituhumu Saudi Arabia kwa kuzidisha chuki na wasiwasi eneo la Mashariki ya Kati.

Saudi Arabia huongozwa na Wasuni na Iran huongozwa na Washia, na nchi hizo mbili zimekuwa zikiunga mkono pande pinzani katika mizozo ya Syria na Yemen.

Marekani imehimiza kuwepo na utulivu na kuyataka mataifa husika yaendelee na mazungumzo.

Sheikh Nimr al-Nimr aliuawa pamoja na watu wengine 46 Jumamosi baada ya kupatikana na makosa yanayohusiana na ugaidi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kutekelezwa kwa hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh al-Nimr kumesababisha maandamano maeneo ya Washia

Punde baada ya mauaji yake, maandamano yalishuhudiwa maeneo mengi ya Washia.

Ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran ulishambuliwa na kuchomwa moto na waandamanaji.

Baadaye Jumapili, polisi mjini Awamiya alikozaliwa Sheikh al-Nimr katika mkoa wa Mashariki nchini Saudi Arabia walifyatuliwa risasi na watu wasiojulikana.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano ya kupinga Saudi Arabia yanaendelea kuripotiwa Iran

Mtu mmoja aliuawa na mtoto mmoja kujeruhiwa, shirika la habari la Saudi Arabia lilisema.

Polisi wanawasaka washambuliaji, ambao msemaji wa polisi amenukuliwa akisema walitekeleza kitendo cha „ugaidi”.

Waislamu wa dhehebu la Shia wanaoishi mkoa wa Mashariki wamelalamikia kutengwa.