Van Gaal: Tunaweza kuimarika 2016

Man Utd Haki miliki ya picha PA
Image caption Manchester United walikuwa wamecheza mechi nane ligini bila ushindi

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal anaamini wanaweza kutumia vyema ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Swansea Jumamosi na kujiimarisha 2016.

United walikuwa wameenda mechi nane bila ushindi, rekodi yao mbaya zaidi tangu Januari 1990.

"Ni jambo la kufurahisha kwamba unaweza kutekeleza mpango wako kwenye mechi, kwa kuhatarisha, chini ya shinikizo kali,” amesema. “Natumai huu utakuwa mwanzo wa mengi mema mwaka huu.”

Manchester United walifungiwa mabao la kwanza na Anthony Martial kabla ya Gylfi Sigurdsson kusawazishia Swansea.

Lakini nahodha wao Wayne Rooney aliwafungia bao la ushindi dakika 13 kabla ya mechi kumalizika.

Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Rooney kufunga Ligi ya Premia msimu huu lakini lake la 238 kwa Manchester United.

Hii inamuacha akiwa amepungukiwa na mabao 11 pekee kufikia rekodi ya mfungaji bora wa klabu hiyo Sir Bobby Charlton.

"Siku hizi mechi zinazochezwa ni nyingi lakini bado huo ni ufanisi mkubwa,” alisema Van Gaal kuhusu mabao ya Rooney.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rooney akisherehekea kufunga dhidi ya Swansea

“Alifunga bao maridadi, mguu wake wa kushoto ukiwa nyuma ya mguu wa kulia. Huwezi amini.”

United kwa sasa wamo alama tisa nyuma ya viongozi Arsenal, lakini bado wako alama moja chini ya jumla ya alama ambazo mtangulizi wa Van Gaal, raia wa Scotland David Moyes alikuwa amezoa katika hatua sawa msimu aliokuwa nao.