Washirika wa Saudia wavunja uhusiano na Iran

Sheikh al-Nimr Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Washia nchini Bahrain pia waliandamana kupinga kuuawa kwa Sheikh al-Nimr

Washirika kadha wa Saudi Arabia wamejiunga na taifa hilo katika kuvunja uhusiano na Iran huku mvutano ukizidi kuhusu kuuawa kwa mhubiri wa Kishia.

Mataifa hayo ni Bahrain, Sudan na Jumuiya ya Milki za Kiarabu (UAE).

Saudi Arabia ilikuwa imewapa wanabalozi wa Iran siku mbili kuondoka nchini Saudi Arabia kufuatia mvutano uliotokana na kuuawa kwa mhubiri maarufu wa Kishia.

Bahrain, ambayo hutawaliwa na Mfalme Msuni lakini raia wengi ni wa dhehebu la Shia, nayo ilifuata wa kuvunja uhusiano.

Ufalme huo pia uliwapa wanabalozi wa Iran saa 48 wawe wameondoka nchini humo.

Sudan nayo ilimfukuza balozi wa Iran kutoka Khartoum huku UAE nayo ikipunguza idadi ya maafisa wa ubalozi. Waislamu wengi nchini Sudan ni Wasuni.

Taarifa ya wizara ya ammbo ya nje ya Sudan imesema: "Kufuatia mashambulio ya kikatili dhidi ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran na afisi yake ya ubalozi Mashhad... Sudan inatakaza kwamba imevunja uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Mhubiri huyo Sheikh Nimr al-Nimr aliuawa pamoja na watu wengine 46 baada ya kupatikana na makosa yanayohusiana na ugaidi.

Washia walishutumu hatua hiyo na maandamano yalishuhudia maeneo yenye Washia wengi.

Mjini Tehran, waandamanaji waliteketeza majengo ya ubalozi wa Saudi Arabia.

Saudi Arabia na Iran ndiyo mataifa makuu ya Kisuni na Kishia mtawalia Mashariki ya Kati, na yamekuwa yakiunga mkono pande pinzani katika mizozo inayoendelea Syria na Yemen.

Kuna wasiwasi huenda machafuko yakatokea kanda hiyo.

Jumatatu, misikiti miwili ya Wasuni ilishambuliwa na imam mmoja akauawa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Misikiti miwili imeshambuliwa nchini Iraq

Saudi Arabia ilitangaza kwamba imekatiza uhusiano wake na Iran baada ya maandamano yaliyotokea ubalozi wake mjini Iran. Ilisema pia kwamba imemwagiza balozi wake arejee nyumbani.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema Saudi Arabia inaendeleza sera ya kuzidisha chuki na makambiliano katika kanda hiyo.

Msemaji wa wizara hiyo Hossein Jaber Ansari alisema Jumatatu kwamba Saudi Arabia inajaribu kusuluhisha matatizo yake ya kinyumbani kwa “kuyatoa nje kwa mataifa mengine”.