Uingereza yamtambua mtu wa IS

Haki miliki ya picha IS Video
Image caption Is waua wanaume watano kwa kosa la kuichunguza Uingereza

Vyanzo vya kiintelijensia nchini Uingereza vimeiambia BBC kwamba vinaamini wamemtambua mwanaume mwenye asili ya nchi hiyo ambaye anaonekana katika mkanda wa video wa hivi karibuni wenye kupigia chapuo propaganda za kundi la kigaidi la wanamgambo wa Islamic State.

Vyanzo hivyo vimemtaja mtu huyo kuwa ni Siddhartha Dhar, ambaye anaaminika alikuwa akiishi Mashariki mwa London. Kwa asili Siddhartha anatajwa kuwa ni Mhindi ambaye aliamua kubadilisha dini yake ya awali na kuwa Mwislamu na inafahamika kuwa baada ya hapo aliamua kuijiunga na kundi lenye msimamo mkali la Al Muhajiroun.

Msemaji wa kundi hilo ameiambia BBC kuwa sauti inayosikika katika mkanda huo wa video haijakosewa asilani, hata hivyo dadake na Siddhartha Dhar amenukuliwa akisema kwamba hana uhakika kwamba sauti hiyo ni ya kaka yake.

Ikumbukwe kwamba mkanda huo wa video unaonesha mauaji ya wanaume watano ambao wanashutumiwa kwa kosa la kuichunguza kwa siri Uingereza.