Mwanamuziki apatikana ameuawa Burundi

Burundi Haki miliki ya picha Getty
Image caption Visa vya watu kuuawa vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara Bujumbura

Mwanamziki mmoja kutoka Burundi amepatikana amefariki katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura baada ya kukamatwa na polisi, hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kundi la wanahabari la SOS.

Taarifa hizo zinasema kwamba mwili wa Pascal Tresor Nshimirimana ulipatikana Jumamosi eneo la Musaga, karibu na gereza kuu la Bujumbura.

Polisi wanasema Pascal alijaribu kumnyang'anya bunduki afisa wa polisi, na akauawa na risasi ililofyatuka kutoka kwa bunduki hiyo kwa bahati mbaya

Bw Nshimirimana alikuwa mmoja wa waandamanaji ambao walipinga muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza

Katika kisa kingine, mwili wa kiongozi wa vijana William Nimubona ulipatakana katika maeneo ya Kavuma jijini Bujumbura.

Hata hivyo, hakuna taarifa huru za kudhibitisha mauaji ya kiongozi huyo.

Bw Nimubona alikuwa kiongozi wa mrengo wa vijana katika chama cha National Liberation Forces (NLF) kinachoongozwa na Agathon Rwasa, kiongozi wa upinzani aliyekubali kuchukua kiti cha naibu wa spika baada ya Rais Nkurunziza kushinda uchaguzi tata wa muhula wa tatu.