Gambia: Wafanyakazi wa kike wajifunike nywele

Jammeh Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jammeh ameongoza Gambia kwa miaka 21

Serikali ya Gambia imepiga marufuku wafanyakazi wa kike kufika kazini wakiwa hawajajifunika nywele.

Kupitia barua iliyofichuliwa na magazeti ya kibinafsi nchini humo, serikali ya nchi hiyo inasema wanawake lazima "wafunge nywele zao na kitambaa'' barua hiyo haikutoa sababu yoyote ya kupiga marufuku.

Mwezi uliopita, Rais wa Gambia Yahya Jammeh alitangaza nchi hiyo yenye Waislamu wengi kuwa jamhuri ya Kiislamu.

Aliongezea kuwa watu wasio Waislamu hawangelazimishwa kuvalia mavazi ya Kiislamu.

Gambia ni maarufu sana kwa watalii kutoka magharibi kutokana na fukwe zake.

Mwaka 2013, Rais Jammeh aliondoa taifa hilo kutoka kwa Jumuiya ya Madola akisema muungano huo wa Uingereza na mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza ni ukoloni mamboleo.