Polisi wasaka washukiwa wanne wa ugaidi Kenya

Bunduki
Image caption Serikali inasema bunduki zilizopatikana zilitumiwa kushambulia maafisa wa usalama awali

Maafisa wa usalama nchini Kenya wanawasaka washukiwa wanne wa ugaidi ambao wanadaiwa kukwepa msako wa polisi katika nyumba moja Mombasa.

Polisi walipata bunduki mbili na vilipuzi baada ya kuvamia nyumba iliyokuwa ikitumiwa na wanne hao Jumatatu.

Kamishna wa jimbo la Mombasa Nelson Marwa anasema bunduki moja iliyopatikana ilitumiwa kumuua afisa wa polisi mjini humo mwaka uliopita.

Image caption Polisi walipata bunduki na silaha nyingine

Bunduki hiyo nyingine aina ya M4 ilitumiwa wakati wa shambulio katika kambi ya jeshi mjini Mombasa mwishoni mwa Novemba.

Polisi wametoa picha za washukiwa hao wanne ambao wanasema ni miongoni mwa kundi la wapiganaji wa al-Shabab waliojificha msitu wa Boni, kilomita 500 kaskazini mwa Mombasa.

Wakati wa msako huo, polisi walipata kitita cha pesa.