Elementi nne zaongezwa mfumo radidia

Kosuke Haki miliki ya picha AP
Image caption Kosuke Morita aliongoza wanasayansi wa Japan waliogundua elemeneti 113

Shirika la Kimataifa la Kemia limeongeza rasmi elementi nne kwenye jedwali la elementi na kujaza mstari wa saba wa kulala kwenye jedwali hilo.

Elementi hizo ndizo za kwanza kuongezwa kwenye jedwali hilo tangu 2011, elementi nambari 114 na 116 zilipoongezwa.

Jedwali kamili la kwanza lilitayarishwa na mwanakemia Mrusi Dmitri Mendeleev mwaka 1869.

Elementi hizo mpya zilithibitishwa na Shirika la Kimataifa la Kemia (IUPAC) tarehe 30 Desemba 2015.

Shirika hilo limetangaza kwamba kundi la wanasayansi kutoka Urusi na Marekani lilikuwa limetoa ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha ugunduzi wa elementi 115, 117 na 118.

IUPAC imesema elementi nambari 113 iligunduliwa na kundi la watafiti wa Japan katika taasisi ya Riken.

Waliogundua elementi hiyo wametakiwa kuwasilisha mapendekezo ya majina ya kudumu na alama za kutumiwa katika sayansi.

"Jamii ya kemia ina hamu sana ya kuona jedwali muhimu la elementi likiwa limejazwa hadi mstari wa saba,” amesema Prof Jan Reedijk, rais wa kitengo kinachoshughulikia kemia isiyo ya viumbe hai katika IUPAC.

Elementi hizo mpya zinaweza kupewa majina ya dhana, madini, pahala au taifa, kampuni au mwanasayansi.

Baada ya majina yatakayowasilishwa na wanasayansi hao kukubalika, yatawasilishwa kwa umma kufanyiwa utathmini. Mwishowe, baraza la sayansi litafanya uamuzi wa mwisho.