Washukiwa wa mapinduzi Burundi warejea kortini

Jenerali Cyriaque Ndayirukiye
Image caption Jenerali Ndayirukiye anasema hajatendewa haki

Watu 28, wakiwemo wakuu za zamani wa jeshi, wanaotuhumiwa kuhusika katika jaribio la kupindua serikali ya Burundi mwezi Mei, mwaka jana wamefikishwa tena kortini Bujumbura.

Washukiwa hao, akiwemo Jenerali Cyriaque Ndayirukiye, wamekataa kujibu mashtaka akisema hajatendewa haki kwenye kes hiyo.

Ameambia mahakama kwamba mawakili wake walizuiwa kumtetea, na pia akaomba washukiwa wengine watatu wafike kortini kutoa ushahidi.

Jenerali Ndayirukiye alikuwa wakati mmoja waziri wa ulinzi.

Watatu hao, ambao Jenerali Ndayirukiye anataka watoe ushahidi, ni Jenerali Gaciyubwenge, aliyekuwa waziri wa ulinzi wakati wa mapinduzi na ambaye sasa yuko uhamishoni, Jenerali Prime Niyongabo, mkuu wa majeshi ambaye bado anaongoza majeshi, na Jenerali Godefroid Niyombare, ambaye ndiye aliyejitangaza mkuu wa mapinduzi hayo ya Mei 13.

Jenerali Niyombare yuko mafichoni na serikali bado inamsaka.

Image caption Washtakiwa wakiwa nje ya mahakama

Washtakiwa wengine, ambao walikuwa maafisa wa jeshi na polisi, wameshtakiwa makosa mengine yakiwemo kujaribu kupingua serikali, kushawishi raia kuchukua silaha, kuua wanajeshi, polisi na raia na kuharibu majumba ya watu.

Mkakosa hayo yana adhabu ya kati ya kufungwa miaka 15 hadi kifungo cha maisha.

Mwendesha mashtaka ameomba washtakiwa wote wahukumiwe kifungo cha maisha jela.