Bomoabomoa yaendelea kutikisa Dar

Baadhi
Image caption Baadhi ya wakazi wameamua kujenga vibanda vya muda juu ya vifusi

Mamia ya watu wameendelea kuathiriwa na zoezi la Serikali la kubomoa nyumba zilizojengwa maeneo hatari au yasiyoruhusiwa jijini Dar es Salaam.

Wakazi wa eneo la Bonde la Mkwajuni, Dar es Salaam ndio wa karibuni zaidi kuathiriwa na zoezi hilo la serikali lililoanza 17 Desemba mwaka jana.

Serikali inasema nyumba hizo ziko katika maeneo ya hatari hasa ikiwa mafuriko yatatokea.

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linasema zoezi hili litalenga kubomoa takriban nyumba 4,000.

Jumanne, kundi la wakazi 680 lilipata afueni baada ya Mahakama Kuu kuamuru serikali kutobomoa nyumba zao kwa muda hadi kesi waliyowasilisha kortini isikizwe na kuamuliwa.

Wakazi hao wa eneo la Bonde la Msimbazi, kupitia wanasheria wao, wanasema kwamba eneo lao halifai kubomolewa nyumba kwa sababu wameendelea kulipa kodi ya viwanja.

Aidha, wanasema wamekuwa wakipokea huduma muhimu kutoka kwa serikali kama vile maji na umeme na wameendelea kuvilipia.

Image caption NEMC imesema nyumba takriban 4,000 zitabomolewa

Wanasema maeneo hayo wameyarithi kutoka kwa wazazi wa wazazi wao.

Nyumba zilizo maeneo yasiyoruhusiwa zimewekewa alama ya ‘X’ kuashiria kwamba zitabomolewa.