Boateng arejea AC Milan

Boateng Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Boateng alisimamishwa kucheza Schalke mwezi Mei mwaka jana

Mchezaji wa kimataifa wa Ghana Kevin-Prince Boateng amerejea katika klabu ya AC Milan ya Italia.

"Kevin-Prince Boateng ametia saini mkataba wa hadi 30 Juni, 2016," klabu hiyo imesema kupitia taarifa.

Kiungo huyo wa kati, 28, alisimamishwa kucheza kwa muda usiojulikana na klabu ya Schalke ya Ujerumani mwezi Mei na amekuwa akifanya mazoezi na klabu hiyo ya Italia tangu Septemba.

Amerejea Italia bila kulipiwa ada yoyote.

Mpango wake wa kuhamia Sporting Lisbon ulitibuka majira ya joto yaliyopita na alisalia kwenye vitabu vya Schalke tangu Desemba.

Schalke walimsimamisha kucheza Boateng baada yao kulazwa 2-0 mjini Cologne, wakisema kulikuwa na kutoaminiana kati ya klabu hiyo na mchezaji huyo.

Boateng alijiunga na Milan mara ya kwanza kwa mkopo kutoka Genoa 2010, na kisha akapata mkataba wa kudumu 2011. Aliwachezea mara ya mwisho Agosti 2013.

AC Milan, watakaokuwa wenyeji wa Bologna uwanjani San Siro Jumatano, wamo nambari sita Serie A, alama nane nyuma ya viongozi Inter Milan.