Shaka kuhusu madai ya bomu Korea Kaskazini

Kiongozi wa Korea Kaskazini Haki miliki ya picha
Image caption Kim Jong Un kiongozi wa Korea Kaskazini

Korea Kaskazini inasema kwa mara ya kwanza imefanikiwa kufanya majaribio ya bomu la nguvu ya maji, maarufu kama bomu la haidrojeni.

Wataalamu hata hivyo wametilia shaka madai hayo, huku mataifa yenye ushawishi duniani yakisema hatua hiyo ya Korea Kaskazini ni uchokozi.

Tangazo hili limetolewa na runinga ya taifa baada ya kusikika mitetemeko ya ardhi ya kipimo cha tano nukta moja, karibu na eneo kuliko na kinu cha nyukilia. Wataalamu wa Marekani wanafanya uchunguzi ikiwa yalikuwa majaribio ya bomu hilo au ilikua zana nyingine ya nyuklia isiyokuwa na nguvu.

Mwandishi wa BBC anasema bomu la nguvu ya maji lina uwezo mkubwa wa mlipuko ikilinganishwa na mabomu mengine yenye madini ya Plutonia ambayo Korea kaskazini imefanya majaribio katika miaka ya awali.

Baadhi ya wataalamu wanasema mlipuko uliosikika haukufikia ule unaotokana na bomu la haidrojeni.

Bruce Bennett, mtaalamu katika shirika la Rand Corporation, ni mmoja wa wanaotilia shaka ukweli wa madai ya Pyongyang. Anasema bomu la haidrojeni lingetoa sauti mara 10 kuliko iliyosikika wakati wa mlipuko wa bomu hilo.

Pyongyang imefanya majaribio mengine matatu ya kinyuklia katika eneo kulikofanywa majaribio ya sasa katika kipindi cha miaka kumi. Majaribio ya leo yakithibitishwa, basi itakuwa mara ya nne kwa Korea Kaskazini kufanyia majaribio bomu la haidrojeni tangu 2006.

Image caption Mitetemeko ya ardhi ilisikika karibu na kinu cha Punggye-ri

Korea Kusini imesema tangazo la Pyongyang ni uchokozi lakini ikaongeza kwamba inatilia shaka ukweli wa madai hayo.

Serikali za Marekani, Urusi, Uchina zimeshutumu habari hizo, pamoja na Muungano wa Ulaya (EU) na shirika la kujihami la mataifa ya Magharibi, Nato.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepangiwa kufanya mkutano wa dharura baadaye Jumatano.