Wafungwa wawili wa Guantanamo wapelekwa Ghana

Guantanamo Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wafungwa 105 bado wanazuiliwa Guantanamo

Wafungwa wawili waliokuwa wakizuiliwa katika gereza la Guantanamo Bay, Cuba, wamehamishiwa Ghana.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema idhini ilitolewa kwa Khalid al-Dhuby kuachiliwa huru 2006 na kwa Mahmoud Omar Bin Atef mwaka 2009.

Wawili hao, wanaotoka Yemen, wamezuiliwa kwa zaidi ya mwongo mmoja na hawajawahi kufunguliwa mashtaka.

Ghana imetoa idhini kwa wawili hao kukaa nchini huko kwa miaka miwili, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ghana Hanna Tetteh amesema.

Kwa mujibu wa stakabadhi za jeshi la Marekani, Mahmoud Omar Bin Atef ni raia wa Yemen aliyezaliwa Saudi Arabia mwaka 1979 .

Alikamatwa nchini Afghanistan 2001.

Khalid al-Dhuby naye ni mzaliwa wa Saudi Arabia, aliyezaliwa in 1981 na kwenda Afghanistan kupigana.

Taifa hilo la Afrika Magharibi hawalijawahi kuwapokea wafungwa kutoka Guantanamo awali.

Nchi kadha zimewapokea wafungwa wa zamani wa Guantanamo, zikiwemo Uganda na Cape Verde.

Watu 780 walizuiliwa Guantano tangu 2002, lakini kwa sasa ni 105 pekee waliosalia gerezani. Hamsini kati ya hao wameidhinishwa kuachiliwa huru.

Jela hilo ilijengwa na Marekani baada ya amshambulio ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001 na hutumiwa na Washington kuwazuilia „wapiganaji maadui”.

Rais Barack Obama amesema anataka kufunga gereza hilo kabla ya kuondoka madarakani mapema 2017.