Zawadi ya jackpot ya £50.4m yakosa mshindi

Zawadi Haki miliki ya picha PA
Image caption Sasa mshindi lazima ajulikane Jumamosi

Zawadi ya jackpot ya £50.4m ilikosa mshindi Jumatano kwenye droo ya shindano la bahati nasibu la kitaifa nchini Uingereza.

Sasa droo nyingine itafanyika Jumamosi kutafuta mshindi au washindi wa fedha hizo.

Ni lazima mshindi apatikane au kuwe na watu watakaogawana zawadi hyo Jumamosi, waendeshaji wa shindano hilo Camelot wamesema.

Nambari zilizokuwa na ushindi Jumatano baada ya droo kufanywa 20:30 GMT (saa tano unusu usiku Afrika Mashariki) zilikuwa 8, 30, 40, 50, 54, 57 nao mpira wa bonasi ukiwa nambari 13.

Lakini hakuna aliyekuwa na mseto huo wa nambari.

Tovuti ya uuzaji tiketi ilikwama mwendo was aa 18:00, na wanunuzi hawakuweza kununua tiketi kwa kipindi cha dakika 10 hivi.

Camelot wamesema walikuwa wakiuza tiketi kwa kasi ya 200 kila sekunde saa moja kabla ya uuzaji wa tiketi kufungwa saa 19:30 GMT.

Jackpot kubwa zaidi kuwahi kushindaniwa awali ilikuwa £42m, ambayo mwishowe iligawanwa na washindi watatu Januari 1996.

Jackpot hii ya sasa inatokana na kuendelezwa mara 13 mtawaliwa kwa shindano na hii ni baada ya idadi ya mipira kwenye droo kuongezwa kutoka 49 hadi 59 mwezi Oktoba.

Hii ilipunguza uwezekano wa mchezaji kupata nambari zote sita sawa kutoka kwa moja katika 14 milioni hadi moja katika 45 milioni.

Lakini Camelot wanasema mabadiliko hayo yameongeza uwezekano wa mtu kuwa milionea.