UN kuichukulia hatua Korea Kaskazini

Haki miliki ya picha APTN
Image caption Tangazo kuhusiana na jaribio hilo la bomu la Hydrogen la Korea Kaskazini

Siku moja baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la bomu la haidrojeni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubaliana kuanza mikakati ya kuiwekea vikwazo.

Hata hivyo baadhi ya Wataalamu wameonyesha kuwa na wasi wasi kuhusu jaribio la sasa la nyuklia la Korea Kaskazini ambalo ni la nne katika mwongo mmoja, wakisema huenda lisiwe la haidrojeni kutokana na mlipuko uliotokea.

Bomu la hydrojeni ni moja ya mabomu hatari ya jamii atomiki au nyuklia yenye nguvu zaidi. Wataalam wanasema bomu hili la hydrojeni lina uwezo mkubwa kiasi kwamba linaweza kulipua mji mmoja wote kwa mlipuko mmoja.

Kufuatia jaribio hilo jamii ya kimataifa imendelea kulaani tukio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Mambo ya nje ya Korea Kusini Ban Ki moon akisema jaribio hilo la bomu la nyuklia ni hatua ya kuogopesha.

"Hili jaribio kwa mara nyingine limekiuka maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na wito wa pamoja wa jamii ya kimataifa kukomesha vitendo hivyo. Pia linakwenda kinyume kabisa na utamaduni wa kimataifa wa majaribio ya mabomu ya nyuklia. Tendo hilo linaonekana ni la kuogopesha kwa usalama wa kanda na kupuuza juhudi za kimataifa za kuacha kutengeneza silaha za nyuklia. Ninalaani kwa nguvu jambo hilo."

Haki miliki ya picha

Huko Marekani nayo Ikulu ya White house imesema utafiti wake wa awali kuhusu jaribio hilo la bomu nyuklia la Korea ya Kaskazini hauthibitishi madai kwamba nchi hiyo imefanikiwa kulipua bomu la haidrojeni.

Msemaji wa White house Josh Earnest amesema Korea ya Kaskazini inafaa kutengwa zaidi kama itaendelea na matendo yake ya ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa kuhusu silaha za nyuklia ikiwa ni pamoja na kufanya majaribio makombora ya angani.

"Tumesikitishwa sana na matokeo ya uharibifu wa amani na utulivu baada ya matendo ya ukiukaji wa Korea Kaskazini kuzidi kuongezeka. China na Urusi nao pia wamesikitishwa. Ndio maana tunafanya bidii kuiweka pamoja jamii ya kimataifa na kuweka wazi kwa Korea Kaskazini kwamba njia ni moja tu iliyobaki ambayo ni nzuri kwa raia wa Korea Kaskazini, ambayo itakuwa nzuri kwa uchumi wa Korea kaskazini, nzuri kwa nchi Korea Kaskazini kwa maana ya uwezo wao wa kujihusisha na jamii ya kimataifa."