‘Watu wengi’ wauawa kituo cha mafunzo Libya

Watu wengi wameuawa baada ya lori lililokuwa limetegwa bomu kulipuka katika kituo cha kuwapa mafunzo maafisa wa polisi katika mji wa Zliten, magharibi mwa Libya.

Mkazi wa Zliten ameambia BBC kwamba kulikuwa na makurutu 400 waliokuwa wakipokea mafunzo katika kituo hicho mlipuko ulipotokea.

Lori hilo lilikuwa la kubeba maji.

Haijabainika iwapo lililipuka langoni ama lililipuka ndani ya kituo hicho.

Meya wa Zliten Miftah Lahmadi anasema watu 40 wamefariki.

Majeruhi kwa sasa wanapelekwa hospitali zilizoko mji mkuu Tripoli kwa sababu hospitali ya Zliten imelemewa na majeruhi.

Shirika la habari la AFP linasema shirika la habari linalotii serikali iliyoko Tripoli linasema idadi ya waliofariki ni zaidi ya 50 na kwamba watu 127 wamejeruhiwa.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler, amesema shambulio hilo lilikuwa la kujitoa mhanga.