Somalia yatimua wanabalozi wa Iran

Sheik Nimr Haki miliki ya picha AP
Image caption Sheikh Nimr al-Nimr aliuawa baada ya kupatikana na makosa yanayohusiana na ugaidi

Somalia imetangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran ikiituhumu kwa kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.

Serikali ya Somalia imewapa maafisa wote wa ubalozi wa Iran mjini Mogadishu muda wa saa 72 (siku tatu) wawe wameondoka nchini humo.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya mkutano wa baraza la mawaziri wa Somalia.

“Hatua hii imechukuliwa baada ya kutathminiwa kwa kina na kutokana na hatua ya Jamhuri ya Iran kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya Somalia,” taarifa kutoka wizara ya mashauri ya kigeni ya Somalia imesema.

"Jamhuri ya Somalia inaitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuheshimu uhuru wa mataifa yote kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Vienna kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia wa mwaka 1961 na tamaduni za uhusiano wa kidiplomasia.”

Ingawa taarifa hiyo haijaeleza wazi, hatua hiyo inaonekana kuwa na uhusiano na mvutano ambao umesababishwa na mauaji ya mhubiri wa Kishia nchini Saudi Arabia.

Somalia ni moja ya mataifa ambayo yalikuwa yameunga mkono hatua ya Saudi Arabia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran baada ya ubalozi wa Saudia mjini Tehran kushambuliwa mjini Tehran.

Ubalozi huo ulichomwa moto na watu waliokuwa wakilalamikia kuuawa kwa mhubiri huyo Sheikh Nimr al-Nimr Jumamosi iliyopita.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran ulichomwa moto na waandamanaji

Mataifa mengine washirika wa Saudi Arabia kama vile Bahrain, Sudan na Kuwait yaliifuata Saudia katika kuvunja uhusiano wake na Iran.

Djibouti pia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran ikionyesha kuunga mkono Saudi Arabia.

Alhamisi, Iran ilisema Saudi Arabia ilishambulia ubalozi wake mjini Sanaa, Yemen.

Iran na Saudi Arabia zimekuwa zikiunga mkono makundi pinzani katika mizozo inayoendelea nchini Syria na Yemen.