Wapalestina wanne wauawa Ukingo wa Magharibi

Israel Haki miliki ya picha AP
Image caption Israel imesema walijaribu kuwashambulia wanajeshi

Wapalestina wanne wameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kujaribu kuwadunga visu wanajeshi wa Israel katika visa viwili tofauti, jeshi la Israel limesema.

Visa hivyo vilitokea eneo la Ukingo wa Magharibi.

Watatu waliuawa katika makutano ya barabara ya Gush Etzion, ambako visa kama hivyo vimewahi kutokea awali. Wa nne aliuawa karibu na Hebron, jeshi limesema.

Hakuna mwanajeshi aliyejeruhiwa.

Maafisa wa afya wa Palestina wamethibitisha vifo hivyo.

Vyombo vya habari Palestina vimetaja watatu hao kuwa Muhanad Kawazbeh, 20, Ahmed Kawazbeh, 21, na Alaa Kawazbeh, 20, wote kutoka kiji cha Sair, kaskazini mashariki mwa Hebron.

Wa nne ni Khalil Shalalda, 16, pia kutoka Sair.

Kumekuwa na ongezeko la visa vya mashambulio kati ya Waisraeli na Wapalestina miezi ya hivi karibuni.

Waisraeli 22 na Wapalestina zaidi ya 140 wameuawa tangu 1 Oktoba.

Waisraeli hao wameuawa kwa kudungwa visu, kupigwa risasi na kugongewa magari.

Nusu ya Wapalestina waliouawa wamedaiwa na Israel kuwa washambuliaji. Wengine wameuawa kwenye makabiliano na maafisa wa usalama.