Mshukiwa mwingine wa ugaidi akamatwa Mombasa

Shosi
Image caption Bw Shosi anazuiliwa maafisa wa polisi wakiendelea na uchunguzi

Mshukiwa mwingine wa ugaidi amekamatwa eneo la Mombasa nchini Kenya.

Ikrima Mohammed Shosi alinaswa asubuhi ya leo baada ya kuhusishwa na kundi la kigaidi la al-Shabab kutoka Somalia.

Ikrima Mohammed Soshi aliwekewa mtego na maafisa wa polisi na kukamatwa katika klabu moja mashuhuri mjini Mombasa.

Amewekwa rumande huku uchunguzi ukiendelea kuhusu uhusiano wake al-Shabab.

Taarifa za mahakama zinaonyesha kuwa anashukiwa kuwahifadhi magaidi wa al-Shabab nyumbani kwake.

Anashukiwa pia kwa kupanga kufanya mashambulizi jijini Mombasa, na pia kuwaua maafisa wa usalama. Maafisa wa usalama wanasema huenda alihusika katika mauaji ya kachero mmoja mjin Mombasa mwaka jana.

Polisi wanaamini Ikrima Mohammed Soshi ni nduguye Ishmael Mohammed Soshi, mshukiwa anayesakwa vikali na maafisa wa polisi

Bw Mohammed Soshi anadaiwa kuwa mmoja wa washukiwa wanne waliokuwa wakiwindwa na polisi waliovamia nyumba moja mtaa wa majengo, Mombasa Jumanne.

Polisi walipata bunduki mbili, risasi na vilipuzi kwenye operesheni hiyo.