Kiir awafuta wakuu wa polisi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Sudan kusini Salva Kiir awafuta kazi wakuu wa polisi

Rais wa Sudan kusini Salva Kiir amewafuta kazi majenerali kadha wa polisi wakiwemo mkuu wa polisi na naibu wake.

Hatua hizo zinakuja baada ya bwana Kiir kukubali kutoa wizara ya mambo ya ndani, ambayo inahusika na masuala ya polisi kwa waasi kama sehemu ya makubaliano ya amani.

Nafasi za mkuu wa polisi Pieng Deng Kuol na naibu wake Andrew Kuol Nyuon zimechukuliwa na Makur Arol na Biel Ruot mtawalia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Salva Kiir na Riek Machar

Pande zote mbili zilifanya mazungumzo katika mji mkuu Juba, ambapo ziliafikia makubaliano ya kugawana mamlaka katika serikali mpya ya umoja.

Serikali ilipata wizara 16 ikiwemo wizara ya fedha na usalama wa kitaifa huku waasi wakipata wizara 10 ikiwemo ya mafuta, ya ndani na ya masuala ya kibinadamu.

Wafungwa wa zamani wa kisiasa walipewa wizara za masuala ya kigeni na uchukuzi huku vyama vya upinzani vikipewa wizara za masuala ya baraza la mawaziri na kilimo.

Mzozo ulianza mwaka 2013 katika taifa hilo changa zaidi duniani wakati bwana Kiirr alimfuta kazi makamu wake wa rais Riek Machar kwa kupanga mapinduzi.