Wanafunzi warejea chuo kikuu Garissa

Garissa
Image caption Chuo cha Garissa kilifunguliwa rasmi Jumatatu iliyopita

Wanafunzi wamerejea tena katika Chuo Kikuu cha Garissa na kuanza masomo miezi tisa baada ya chuo hicho kufungwa kutokana na shambulio la al-Shabab.

Serikali inasema imeweka usalama wa kutosha kuhakikisha kundi hilo kutoka Somalia haliwezi likashambulia tena.

Licha ya hakikisho kutoka kwa maafisa wa usalama, ni wanafunzi wachache pekee waliorejea chuoni, wengi wao wakiwa wa kujilipia.

Takriban wanafunzi 800 wa kufadhiliwa na serikali, waliokuwa wakisomea katika chuo hicho kabla ya shambulio kutokea, walihamishiwa chuo kikuu cha Moi mjini Eldoret.

Image caption Masomo yameendelea licha ya wanafunzi kuwa wachache

Watu 148 waliuawa kwenye shambulio hilo la al-Shabab lililotekelezwa tarehe 2 Aprili.

Kituo cha polisi kimejengwa ndani ya chuo kudumisha ulinzi.

Maafisa zaidi ya 20 wa polisi watakuwa wakikaa humo.